Kilimo cha bamia sehemu ya pili (02)

Matunzo ya shamba baada ya kupanda
Matunzo ya shamba ni muhimu sana kwa sababu huamua kiasi cha mavuno unayoweza kupata kutoka shambani. Shamba ambalo halipati matunzo mazuri hata kama mbegu bora inayozaa sana itatumika mavuno bado yatakuwa hafifu. Matunzo ya shamba hujumuisha;

Umwagiliaji

Njia za umwagiliaji
Kuna njia tofauti za umwagiliaji ambazo zinaweza kutumika katika umwagiliaji wa bustani ya bamia kama vile umwagiliaji wa njia ya matone (drip irrigation), wa njia ya mifereji na umwagiliaji wa kutumia cane. Kwa kilimo cha kiangazi au pale mvua zinapokuwa hafifu ni muhimu kufanya umwagiliaji wa bustani yako ili kuepuka kunyauka kwa mazao shambani kutokana na upotevu mkubwa wa maji. Wakati wa kumwagilia hakikisha haumwagii maji katika majani bali katika shimo chini ya kichaka cha mche (canopy).

Ratiba ya umwagiliaji
Unaweza kumwagilia bustani ya bamia kila baada siku mbili hadi tatu kutegemeana na hali ya hewa na udongo. Cha msingi usiache udongo ukauke bali mwagia maji angalau asilimia hamsini ya unyevu wa udongo unapokuwa umepotea.

Mambo ya kuzingatia
Ni vyema umwagiliaji wa bustani uzingatie hatua za ukuaji wa mimea bustanini, hali ya hewa na uwezo wa udongo kutunza maji. Mahitaji ya maji kwa zao la bamia huongezeka wakati wa kutoa maua na kutengeneza matunda. Vilevile katika maeneo yenye hali ya joto na udongo wa kichanga maji hupotea kwa urahisi. Hakikisha maji hayatuami katika shamba lako kuepuka kuoza kwa mizizi na udongo haukauki.

Kupunguzia
Ng’olea miche katika shamba wakati wa kufanya palizi ya kwanza wiki nne tangu  kupanda ikiwa na urefu wa sm 10 hadi 15.  Bakiza mmea mmoja wenye afya katika kila shimo. Mimea iliyong’olewa kutoka katika shimo moja inaweza kupandikizwa katika shimo lingine ambalo mbegu hazikuota.

Kuweka Mbolea
Weka mbolea ya kukuzia aina ya Urea wiki sita tangu kupanda kwa kiwango cha nusu kizibo cha soda kuzunguka shina sm 5 kutoka shina lilipo na kurudia kuweka tena kila baada ya wiki mbili hadi mwisho wa kuvuna. Mmea unapokuwa mkubwa wenye majani mengi usiweke mbolea ya kukuzia hadi bamia zitakapo toka vinginevyo mmea unaweza kuwa na majani mengi na kuzaa bamia chache. Mfuko mmoja wa Urea wa kilo 50 unatosha kutumika katika eneo la ekari moja.

PITIA
JINSI YA KUDHIBITI VIWAVIJESHI KWA KUTUMIA VIUTILIFU.

Kupiga Dawa
Dawa za ukungu
Uchaguzi wa dawa za ukungu hufuatana na magonjwa yanayoshambulia zao husika hivyo ni vema kujua magonjwa yanayoshambulia zao la bamia kabla ya kuchagua dawa za kutumia kama kinga au tiba pale magonjwa yanapojitokeza.  Unaweza kuanza kupiga dawa ya ukungu wiki moja hadi mbili tangu miche kuota na kurudia kila baada ya wiki moja hadi mbili kutegemeana na maelekezo ya dawa husika.

Dawa za kuua wadudu
Nyunyizia dawa ya kuua wadudu baada ya kuona wadudu waharibifu katika shamba lako ili kuweza kuchagua dawa sahihi ya kudhibiti aina ya wadudu waliovamia bustani yako.

Kupalilia
Palizi ifanyike kuanzia wiki ya nne tangu kupanda na kurudia kila baada wiki mbii hadi tatu. Hakikisha hakuna magugu bustanini katika kipindi cha kutoka maua na kutengenezwa kwa matunda. Unaweza kupalilia kwa kutumia mikono, jembe dogo la mkono au dawa za viuagugu zinazopatikana katika maduka ya pembejeo za kilimo.  Fuata ushauri wa wataalamu walio katika eneo lako na maelezo ya dawa kama yalivyo kwenye lebo ya chupa.

Kuweka Matandazo
Matandazo husaidia kudhibiti magugu, kuifadhi unyevu na kuongeza rutuba katika udongo. Kwa matokeo mazuri katika udhibiti wa magugu inashauriwa kuweka matandazo kwa kuyatandaza katika udongo katika kina cha sm 10 mpaka 15 maeneo yote ya tuta kuzunguka mashimo ya miche. Matandazo ya asili kama mabua ya nafaka, pumba za mpunga, maganda ya karanga na maranda ya mbao yanaweza kuwekwa kabla ya kupandikiza baada ya kuchimba mashimo ya kupandia au baada ya kupandikiza. Matandazo ya plastiki huwekwa mapema kabla ya kupandikiza baada ya kuandaa matuta.

PITIA
NUFAIKA KWA KILIMO BORA CHA DENGU

KUVUNA
Kiwango cha mavuno
Kiwango cha mavuno ya bamia kwa ekari moja hutegemeana na matunzo ya shamba, uwezo wa kuzaa wa mbegu iliyotumika na idadi ya mimea katika shamba. Mbegu za aina tofauti zina uwezo tofauti wa kuzaa na hivyo mavuno huwa tofauti. Vilevile mashamba tofauti yaliyopandwa mbegu ya aina moja na kupata matunzo ya viwango tofauti huwa na kiwango tofauti cha mavuno. Kwa bustani ya bamia iliyopandwa mbegu bora na kutunzwa vizuri huweza kutoa mavuno wastani wa tani 5 hadi 8 kwa ekari.

Muda wa Kuvuna
Bamia huchukua siku 50 hadi 60 kuanza kuvuna. Huwa tayari kuvunwa siku tano tangu kutoka kwa maua zikiwa bado changa na zenye urefu wa sm 5 hadi 10 kutegemeana na aina ya mbegu. Hivyo basi inashauriwa kuvuna bamia kila baada ya siku tatu tangu mvuno wa kwanza wakati wa asubuhi. Uvunaji wa bamia unaweza kuendelea kwa muda wa siku 30 hadi 40 tangu mvuno wa kwanza.

Namna ya uvunaji
Mambo ya kuzingatia
Usiache bamia zikomae kabla ya kuvuna kwa sababu bamia zilizokomaa huwa ngumu na zenye nyuzi nyuzi na hivyo hazina soko kwa matumizi ya nyumbani.Vilevile kuacha bamia zikomae katika mmea husababisha mmea kuacha kuzaa mapema na hivyo mavuno huwa madogo.

Tumia kisu au mkasi wakati wa kuvuna ili kuepuka kuathiri shina na kusumbua mizizi ya mmea. Vilevile usivune bamia zinazoonyesha dalili ya kuoza au kuathiriwa na wadudu. Kwa baadhi ya watu bamia huweza kusababisha muwasho wa ngozi hivyo hakikisha unavaa suruali ndefu na shati la mikono mirefu wakati wa kuvuna.

Hatua za uvunaji
Hatua zifuatazo zinaweza kutumika katika uvunaji;
Andaa vifaa na vyombo vya kuvunia kama vile kisu, mkasi na ndoo au chombo chochote cha plastiki kwa kuvisafisha kwa maji safi na sabuni. Andaa sehemu utakayokuwa unaweka bamia wakati wa kuvuna iliyo kivulini karibu na shamba na utandike turubai.

PITIA
KANUNI SAHIHI ZA KILIMO BORA CHA MCHICHA

Wakati wa kuvuna kata kikonyo cha bamia karibu na tawi linaloshikilia tunda kisha weka tunda kwenye ndoo. Hakikisha unavuna bamia na kikonyo chake ili zisiharibike kwa urahisi.

Ndoo inapojaa bamia beba ukazitandaze katika turubai lililo tandikwa karibu na bustani ili zipate hewa na zipoe kutoka katika joto la shamba (field heat) kabla ya kuzipakia.

Safisha vizuri vyombo vya kuvunia kwa maji safi na sabuni kila baada ya kumaliza siku ya kuvuna ili kuzuia vimelea vya magonjwa.
bamia zilizochumwa

Bamia zilizochumwa
Matunzo baada ya kuvuna

Kupakia
Baada ya kuvuna pakia bamia kwenye matenga au makreti yaliyo tengenezwa kwa mbao au plastiki yenye matundu yanayo pitisha hewa vizuri. Hakikisha upakiaji unafanyika kivulini ili bamia zisiunguzwe na jua.

Kuhifadhi
Bamia huweza kuifadhiwa katika chumba maalum cha kuifadhia (cold room)  katika nyuzi joto za sentigredi 7˚C hadi 10˚C na unyevu hewa 95% na kukaa bila kuharibika kwa muda wa siku saba hadi kumi. Vilevile unaweza kuifadhi bamia katika chumba chochote kisafi kikubwa chenye nafasi na kisicho na joto jingi chenye madirisha yanayo pitisha hewa vizuri, feni au Air conditioner kwa kupanga matenga kwa nafasi bila kuyarundika sehemu moja.

Mambo ya kuzingatia
Bamia huweza kuharibika kwa haraka baada ya kuvunwa hivyo ni muhimu kuhakikisha haziifadhiwi kwa muda mrefu na zinafika sokoni mapema baada ya kuvunwa. Jambo hili litawezekana kwa urahisi ikiwa mkulima atahakikisha soko linakuwa tayari kabla ya kuanza uvunaji.

Somo letu la bamia limeishia hapa. Asante kwa kusoama makala haya.

Jiunge Nasi Telegram

Usipitwe na Nyaraka mpya kila zikiwekwa kwenye Tovuti yetu na weza kujifunza kwa kina ukitumia simu. Jiunge sasa hapa.

Kilimo bora cha Ndizi

Hapa Tanzania kilimo cha migomba kimekuwepo Kwa miaka mingi. Kilimo hiki ni maarufu sana kwa sababu zao la ndizi limekuwa likitumika kama chakula kikuu kwa

Read More »

UFAHAMU MFUMO WA KILIMO SHADIDI

Mfumo wa kilimo shadidi cha mpunga (MKiShaMpunga) unaojulikana kwa Kimombo kama ‘Sytem of Rice Intensification’ au ‘SRI’ kwa ufupi unajumuisha mbinu  vumbuzi za kilimo ambazo

Read More »